by EAGMA
15 Apr, 2025
BASATA NA EAST AFRICA GOSPEL MUSIC AWARDS WAFANYA KIKAO CHA KIMKAKATI CHA KUSUKUMA SANAA YA INJILI!
Leo, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana, amekutana na Mkurugenzi wa East Africa Gospel Music Awards (EAGMA), Bi. Magreth Chacha, katika ofisi za BASATA kwa ajili ya kikao cha kimkakati cha kuboresha na kuendeleza sekta ya muziki wa injili katika ukanda wa Afrika Mashariki. Katika kikao hicho, pande zote mbili zilijadili kwa kina mbinu na mikakati ya kuimarisha na kukuza muziki wa injili kupitia East Africa Gospel Music Awards. EAGMA imejizatiti kutoa tuzo na kuhamasisha wanamuziki wa injili katika kukuza talanta zao na kufikia hadhira kubwa zaidi. Bi. Magreth Chacha alieleza mipango ya EAGMA kuendeleza na kutoa jukwaa la kipekee kwa wasanii wa muziki wa injili katika kanda ya Afrika Mashariki. Vilevile, Dkt. Mapana alisisitiza umuhimu wa BASATA kushirikiana na tuzo hizi ili kuhakikisha muziki wa injili unapata nafasi stahiki katika tasnia ya muziki nchini na kimataifa. Katika kikao hicho, BASATA ilijizatiti kuandaa mikakati ya kusaidia wanamuziki wa injili kuungana na wasanii wa kimataifa na kuhakikisha wanapata nafasi za kuonyesha talanta zao kwenye majukwaa makubwa. Pamoja na hili, Dkt. Mapana alitoa wito kwa wasanii wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi katika mashindano ya EAGMA ili kufikia mafanikio makubwa katika sekta ya muziki. BASATA na EAGMA watashirikiana kwa karibu ili kuona muziki wa injili unapata nafasi kubwa zaidi, ukiwa na athari chanya kwa jamii na tasnia ya muziki kwa ujumla.